Hotuba ya Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na VVU wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani Dec 1, 2017

uploaded 04/12/2017

 

 

 

 

 

 

 

BARAZA LA WATU WANAOISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI TANZANIA (NACOPHA)

 

SALAMU ZA MWENYEKITI WA NACOPHA KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI 1/12/2017

MNAZI MMOJA JIJINI DAR ES SALAAM

 

Mheshimiwa Mgeni rasmi:      Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,   Mheshimiwa  Samia Suluhu Hassan  

Mheshimiwa:                           Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda

Mheshimiwa:                           Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ;Sera, Bunge, Kazi ,Vijana, Ajira na Wenye UlemavuJenista Mhagama

Mheshimiwa                            Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Ummy Mwalimu

Waheshimiwa:                         Mawaziri na Wakuu wa Serikali waliopo hapa   

Waheshimiwa:                         Wabunge

Mheshimiwa:                           Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania

Waheshimiwa:                         Mabalozi

Waheshimiwa:                         Wawakilishi wa Mashirika Mbalimbali ya Kimataifa na Kitaifa

Waheshimiwa:                         Viongozi wa Asasi zisizo za kiserikali

Waheshimiwa:                         Wawakilishi wa Vyama vya Siasa

Waheshimwa:                          Washiriki wa Mashirika na Vyama vya Watu Wanaoishi na VVU na UKIMWI

Waheshimiwa:                         Washiriki wote, Mabibi na Mabwana

 

Itifaki imezingatiwa!

 

 

 

 

 

 

 

MHESHIMIWA MGENI RASMI

Kwa kuwa Ratiba ya leo inanitaka nitoe salamu, Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi MUNGU Mwingi wa Rehema kwa kutukirimia uzima na amani na kuweza kuyafanikisha yote haya yanayotokea leo hapa viwanjani Mnazi Mmoja.

 

Salamu zangu za pili nazipeleka kwako binafsi Mheshimiwa Makamu wa Rais wetu, kwa kukubali kuungana nasi siku ya leo ya kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani. Kukubali kwako kuungana na sisi WAVIU na wadau wengine wote leo ni heshima ya juu uliyotupatia.  Pia hii ni ishara dhahiri ya kwa  juhudi za Mheshimiwa rais wetu Dr. John Pombe Magufuli  za kuwa na Tanzania tunayoitamani sote ya viwanda visivyozalisha maambukizo mapya ya VVU, Unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na VVU,  na vifo vitokanavyo na UKIMWI ili kuufikia uchumi wa kati.

 

Salamu za tatu zimwendee Mkuu wa Mkoa  wa Dar es salaam, Mheshimiwa Paul Makonda kwa  kukubali kuwa mwenyeji kitaifa kwa maadhimisho  ya siku ya UKIMWI  Duniani kwa mwaka huu wa 2017. Dar es Salaam isiyo na UKIMWI inawezekana kwa ubunifu tunaohushuhudia kwa Mkuu wetu wa Mkoa kujali afya za wakazi wa Mkoa wa Dar es Salamu na majirani zake. Ni hivi majuzi tumeshuhudia upimaji mkubwa wa afya bure hapa Bandarini kwa msaada wa Watu wa China ukihamashishwa na Mkuu wa Mkoa wetu.

 

MHESHIMIWA MGENI RASMI

Kwa heshima kubwa,  napeleka salam nyingi kwa WAVIU wote walioweka hali zao wazi kuwa wanaishi na VVU pamoja na wale ambao bado wanatafakari.  Katika watanzania wotw waliojitokeza kupima na kutambua kuwa wanaishi VVU,  takribani watu 616, 984 ni wanachama wa Baraza. Wanachama hawa wa Baraza wako katika  Konga za WAVIU ( Mabaraza ya wanaoishi na VVU) katika Wilaya/Halmashauri 154 za Tanzania Bara. Kuanzishwa kwa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU na Konga zake, kumekuwa ni chachu kubwa dhidi ya mapambano ya kuondoa unyanyapaa dhidi ya WAVIU na UKIMWI ili Watanzania wote walioambukizwa: watoto, vijana na watu wazima wajitokeze na kupata huduma sitahiki ambazo serikali yako inazigharimia kwa gharama kubwa na zinatolewa bure. WAVIU wamekuwa mstari wa mbele kuhamashisha jamii yote kupima na kuweka wazi hali zao za  afya ili kupata huduma zinazotolewa na serikali yako.

 

 

MHESHIMIWA MGENI RASMI

 

Ujumbe wetu leo Kwa Serikali ya Awamu ya Tano:

Kwa kuzingatia  dhamira ya taifa ya kuyafikia malengo ya kimataifa ya taifa ya 90 90 90: Tunapenda kuipongeza serikali yetu  ya awamu ya tano kwa kutujali sana WAVIU na afya za Watanzania kwa ujumla. Tunapongeza pia uamuzi wa  serikali  kuongeza Bajeti ya Afya  kwa kiwango kikubwa katika awamu hii ya tano na hasa ikizingatia tiba na Kinga dhidi ya maambukizi ya VVU.

 

 

 

Kupitia chombo chetu (Baraza), tunaunga Mkono juhudi hizi kwa kushiriki  katika programu mbalimbali  kama vile kuelimisha jamii juu ya kujikinga na maambukizi ya VVU, Tiba na matunzo, ufuasi sahihi wa tiba,  kupiga vita unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na VVU na UKIMWI, kuhamasisha na kuhimiza  ushirikishwaji wa dhati wa watu waishio na VVU na UKIMWI  katika utengenezaji na utekelezaji wa sera, mipango na program mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kutetea na kupigania kuwezesha asilimia 73.4 ya tuliowafikia kupima na kupata majibu yao. Pia tumeweza kuwarudisha kwenye tiba kwa asilimia 92 ya wale wote tuliowafikia. Kupitia vikundi vyetu wezeshi takribani asilimia 89% wanajishugulisha na shughuli za kiuchumi, wengi ni wanawake. Haya ni mafanikio makubwa  yaliyotokana na Ushiriki Mkubwa wa WAVIU katika utoaji huduma  na kupiga vita Unyanyapaa japo changamoto  bado ipo kwa vijana na  wengi walio kwenye umri ulio chini ya miaka 24. Lakini tumedhamiria kusshghulka na changamoto hii.

 

MHESHIMIWA MGENI RASMI

Pamoja na jitihada hizi za serikali, bado kuna changamoto  mabali mbali ikiwemo uhaba wa dawa za magonjwa nyemelezi, na zinakopatikana zinauzwa. Uwezo wa WAVIU wengi kununua dawa hizi kila mara ni mdogo mno, hivyo tunashindwa kuzipata na hivyo kuathiri afya zetu na hata kufa. Tunaomba WAVIU wote kuwekwa kwenye mpango wa bima ya afyaili kurahisisha upatikanaji wa huduma hii kwa urahisi.   Pia nashauri Dawa za ARV ziundiwe sheria ili kuwabana wale wanaoacha na kuzitumia  vibaya kwani serikali inatumia gharama kubwa.

 

Huduma za tiba za ART bado ziko mbali kwa WAVIU wengi vijijini. Hili linasababisha ufuasi sahihi wa dawa kuwa mgumu kwa wengi wa WAVIU.  Tunaomba serikali ishushe  huduma hii katika ngazi ya jamii ili kuokoa maisha ya WAVIU wengi wanaoacha dawa kwa sababu ya umbali na gharama za kufuata dawa hizo kutoka vituo vya mbali

 

Uangalizi  na huduma za wa watoto wanaioshi na VVU mashuleni uboreshwe ikiwa ni pamoja na kuondoa adha upungufu wa vitendanishi na dawa  za ARV kwa watoto wachanga hadi kufikia umri wa miaka  10  katika baadhi ya vituo jambo linalowalazimu kupewa dawa za watu wazima wakati mwingine.

 

Swala la lishe bora ni swala nyeti sana kutokana na hali ya Afya zetu watu tunaoishi na Virusi vya UKIMWI hivyo basi tunasisitiza WAVIU tuwajibike kwa nafasi zetu na tunaomba MFUKO WA ‘TASAF’ uwahusishe WAVIU pia.

 

Pia tunapongeza agizo  la Mheshimiwa Rais la hivi karibuni juu ya kuhuisha  Viwanda vya Madawa hapa nchini. Tunashauri kuwa ni  vyema kutumia fursa hii kwa mojawapo ya Viwanda hivi au Vyote  kuzalisha Madawa ya Kufubaza VVU . Tunaamini hili litachangia kupunguza mzigo mkubwa wa serikali katika kununua madawa haya kutoka nje ya nchi na kuboresha huduma zingine kwa WVIU na wanachi kwa jumla.

 

 Sasa pia  ni wakati muafaka wa kuhuisha sera ya Taifa ya UKIMWI kwani iliyopo iliundwa mwaka 2001. Sera mpya ni muhimu kwani itatoa msukumo mpya kwa  mwitikio wa kupambana na VVU na UKIMWI  utakaondena na hali ya sasa iliyopo nchini.

 

 

 

 

Ujumbe kwa Mashirika ya Kimataifa na ndani ya Nchi

 Tunatambua na kutoa shukurani kwa michango inayotolewa na Wandau mbalimbali wa maendeleo, yakiwemo mashirika na taasisi za Kimataifa kama vile UNAIDS, PEPFAR, Global Fund,  mashirika na balozi mbali mbali hapa nchini, kwa kufadhili shughuli nyingi na huduma vinazolenga kuondoa maambukizi ya VVU na UKIMWI nchini. Ni dhahiri kuwa uhitaji kwa msaada endelevu  kwa juhudi zilizokwisha anzishwa ni tegemeo letu na kwa kuimarishshaa na kuboresha huduma na mifumo yake pia. Serikali yetu inalo jukumu la kuhakikisha kuwa huduma za afya hususani WAVIU zinabaki kuwa endelevu pale misaada ya nje inapoanza kupunguzwa.   Tunahitaji kushirikiana na vyombo vingine vya kisheria na vyenye mamlaka zaidi ikiwemo Serikali kama inavyozungumzwa kwenye sheria ya UKIMWI (HAPCA 2008) na sera ya Taifa ya UKIMWI.

 

Ujumbe kwa Sekta za Umma na Binafsi na Jumuiya za Kidini

Napenda kutoa rai kwa sekta zote za umma, sekta binafsi, wafanyabiashara,  wanasiasa, viongozi wa dini, taasisi za elimu ya juu na utafiti, na makundi mengineyo ya kijamii, kuihamasisha jamii kupima na kujua hali zao za maambukizi na endapo watabainika kuwa na maambukiziya VVU  kuanza matibabu mara moja na kuwa na ufuasi sahihi wa dawa kila siku, pia kujenga tabia ya kupima idadi ya virusi vilivyo mwilini mwao mara kwa mara.

 

Natoa wito kwa wasomi, matajiri, wanasiasa, Viongozi wa Serikali, Watendaji Wakurugenzi mnaoishi na VVU na kutumia dawa mjitokeze kufanya kazi na Baraza na sisi WAVIU wenzenu ili kwa pamoja tuhamashishe jamii yote kuipata Tanzania ya Viwanda itakayokuwa na wafanyakazi wenye afya na tija.

 

Ujumbe kwa Watu Wote

Hatutaki kumuacha mmoja wetu nyuma: Watanzania wote tuwe mstari wa mbele kwa kupima na kuwa huru na nafsi zetu kwa kutambuaa hali yetu ya maambukizi ya VVU ili kufikia lengo la kutokuwa na maambukizi mapya ya VVU (0) ifikapo 2030. Wote tupime sasa.  UKIMWI haubagui, hauna rangi, hauna cheo, hauna itikadi,  hauna umri n.k. Kila mtu kwa cheo, itikadi, dini, umri, hali yake kiuchumi n.k anao wajibu wa kuhamasika kupima na kujua hali yake kiafya, kupata tiba na kuhamashisha jamii inayomzunguka ili kujikinga na maambukizi mapya. Unyanyapaa dhidi ya WAVIU upigwe vita kwa nguvu zote na kila mmoja wetu popote alipo ikiwa ni  sambamba na kuwepo kauli rafiki wakati wa kupata huduma za afya.

 

 

KAULI MBIU, 2017
Watu tunaoishi na VVU tumefurahishwa sana na kauli Mbiu ya mwaka huu ambayo inalenga kuwa na huduma endelevu zinazotegemea mapato na michango ya watanzania wenyewe badala ya kutegemea zaidi ufadhali kutoka kwa wahisani kwa kauli mbiu inayosema “CHANGIA MFUKO WA UDHAMINI WA UKIMWI KWA HUDUMA ENELEVU“  hii ni kauli inayotupa mwelekeo mpya  katika mwitikio wa UKIMWI hapa nchini,   na hasa tunapoimarisha mifumo yetu kama nchi kupunguza utegemezi kwa wafadhili kwenye mwitikio wa  UKIMWI hapa Tanzanzania. Shime watanzania tuulinde na kuutegemeza mwitio wetu wa UKIMWI sisi wenyewe kwa faida ya taifa letu.

 

 

MHESHIMIWA MGENI RASMI

Tunaishukuru serikali  yetu kupitia Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa kuendelea kuratibu masuala yote ya UKIMWI na kwa kutupatia nafasi sisi watu tunaoishi na VVU kushiriki maadhimisho haya kila Mwaka.

 

Nitumie  nafasi  hii kutoa  shukrani zetu kwa wadau wote ambao wamekuwa wakituwezeshaFkutekeleza shughuli zetu za Baraza hasa serikali ya Marekani kupitia USAID, Mfuko wa dunia wa kudhibiti Malaria, UKIMWI na TB, Familia ya Umoja wa Mataifa  na Halmashauri zote nchini, VYombo Vya habari na Mashirika ya Dini  kwa kuwezesha shughuli za baraza kuimarika.  Nawashukuru tena Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na wale wote waliotuwezesha kushiriki maadhimisho haya.

 

MHESHIMIWA MGENI RASMI

Kwa kumalizia, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru wote waliyoiwezesha  NACOPHA kufikia hadi hapa tulipo. Nitoe rai kwa wadau wote kushirikiana na kuendelea kulitumia Baraza katika kuratibu, kutetea  na kuwafikia WAVIU pale walipo katika mwitikio wa shughuli za UKIMWI.   

 

Kwa pamoja tunaweza kupambana na kuondoa maambukizi mapya na  UKIMWI Tanzania, 2030.

 

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

 

 

Imetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania

  • COAT OF ARM
  • UNAIDS
  • USAID
  • TACAIDS
  • GLOBAL FUND
  • GNP


The National Council of People Living with HIV & AIDS in Tanzania (NACOPHA) Mbezi Beach Area, Block 'F' Plot no. 450/5 Mwai Kibaki Road, Kinondoni District, Dar es Salaam,Tanzania
Copyright © 2019 NATIONAL COUNCIL OF PEOPLE LIVING WITH HIV TANZANIA