The Speech of National Council of People Living with HIV and AIDS (NACOPHA) Chairman on climax of World AIDS Day 1 December, 2013 Dar es Salaam.

uploaded 04/07/2016

BARAZA LA WATU WANAOISHI NA VIRUSI TANZANIA (NACOPHA)

SALAMU ZA MWENYEKITI WA NACOPHA KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI MKOANI DAR ES SALAAM

Tarehe 01/12/2012

 

Mheshimiwa mgeni rasmi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete

Waheshimiwa Mawaziri na Wakuu wengine wa serikali,

Mheshimiwa Mkuu wa mkoa

Waheshimiwa Wabunge

Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania

Waheshimiwa mabalozi

Wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya Kimataifa

Viongozi wa Asasi zisizo za serikali

Wawakilishi wa Vyama watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI

Ndugu Waalikwa, Mabibi na Mabwana,…itifaki imezingatiwa

 

Mheshimiwa mgeni rasmi

Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetuewezesha wote leo kuwa hapa na kujumuika pamoja kuadhimisha siku hii maalumu ya UKIMWI duniani. Pia napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa serikali unayoingoza , pamoja na wewe binafsi kwa kutoa fursa hii muhimu kwetu sisi Baraza la Taifa la Watu tunaoishi na Virusi vya UKIMWIili tuweze kuongea na Umma wa watanzania na wadau wa maendeleo katika maadhimisho haya ya siku ya UKIMWI duniani leo hii.

 

Ikiwa ni miaka 33 tangu juhudi mbali mbali za kudhibiti UKIMWI zilipoanza hapa nchini, mojawapo ya mafanikio mengi na ya kujivunia katika mwitikio wa kitaifa wa kudhibiti UKIMWI , ni kuundwa kwa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na VVU (NACOPHA). Chombo hiki hadi sasa tayari kimeunda Mabaraza (Konga) ya watu wanaoishi na VVU katika halmashauri za wilaya zipatazo 121 nchini kote. Lengo ni kufikia halmashauri zote za wilaya na manispaa nchini ifikapo mwisho wa mwaka 2013. Baraza pia limejenga uwezo, mshikamano na kufanya kazi kwa pamoja na mitandao 11 ya kitaifa ya watu wanaoishi na VVU na kuwa na sauti moja ya kitaifa katika kutetea na kulinda utu,afya na ustawi wa wanaoishi na VVU Tanzania. Kwa rukhsa yako na heshima kubwa, naomba nitumie fursa hii kuwakumbuka wote waliotagulia mbele ya haki kutokana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwani nao walitoa 2

 

mchango wao mkubwa katika kulijenga Baraza. Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani mahali pema peponi, Amina.

Ndugu Mgeni rasmi

Kupitia ofisi yako, na wewe binafsi, naomba kutoa rai na changamoto kwako kuzielekeza halmashauri zote nchini kulitambua Baraza,kufanya kazi na konga (Mabaraza ya watu wanaoishu na Virusi vya UKIMWI katika ngazi ya Halmashauri za wilaya na manispaa), na kutoa mchango wao katika kuimarisha shuguli za Baraza pamoja na Konga zake. Tunatanguliza shukrani zetu kwa kukubaliana na ombi hili.Tunawashukuru na kuwapongeza baadhi ya Halmashauri ambazo tayari zimeanza kufanya kazi na WAVIU bila hata ya kupewa maelekezo yako binafsi na ama kuoitia waraka wa ofisi yako. Ni matumaini yetu kuwa, kupitia kwako na kuiga mfano wako, serikali na halmashauri zote nchini wataheshimu dhamira yako na kutoa mchango wao katika kuimarisha shughuli za Baraza pamoja na Konga zake.

Mheshimiwa mgeni rasmi

Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “TANZANIA BILA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU, BILA VIFO VINAVYOTOKANA NAUKIMWI NA BILA UNYANYAPAA DHIDI YA UKIMWI INAWEZEKANA” Kwa sisi kama Baraza la watu wanaoishi na VVU Tanzania, kauli hii yenye mwelekeo mpya na inaonyesha wapi tulipotoka hasa tulipoanza mapambano ya kudhibiti UKIMWI nchini na changamoto mbalimbali ambazo tumepambana nazo katika kipindi chote hadi leo hii ambako tunatarajia kuiona Tanzania isiyo na maambukizi mapya ya VVU, Tanzania ambayo haitakuwa tena na vifo vitokanavyo na UKIMWI na pia Tanzania ambayo haitakuwa na unyanyapaa dhidi ya wenye maambukizi ya VVU.

Mheshimiwa mgeni rasmi

Tunapenda kukufahamisha kuwa sisi watu tunaoishi na VVU hapa nchini tunajivunia sana mchango wetu katika kutekeleza malengo ya kitaifa kwenye mwitikio wa kitaifa dhidi ya UKIMWI. Baraza limeweza kushiriki katika utetezi wa haki , nafasi na ushiriki wa WAVIU katika ngazi mbali mbali za za maamuzi, kupitia sera, sheria na miongozo ya kitaifa inayogusa WAVIU na watanzania wote kwa ujumla. Mathalani, Baraza limeshirikishwa kikamilifu katika kutengeneza Mkakati wa III wa kitaifa wa kudhibiti UKIMWI utakaozinduliwa leo, Mwongozo wa kitaifa wa kudhibiti unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya UKIMWI, na Mkakati wa sekta ya afya wa Kudhibiti UKIMWI ( ambao mchakato wake unaendelea). Hii ni moja ya hatua muhimu katika mafanikio ya serikali ya kutambua na kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Paris 2000 ya kuwashirikisha kikamilifu watu wanoishi na VVU katika hatua zote za mwitikio wa kitaifa wa kudhibiti UKIMWI. 3

 

Mheshimiwa Mgeni rasmi,

Baraza linayatambua malengo yote yaliyomo kwenye mkakati na tunaomba kukuhakikishia kuwa WAVIU wote katika ngazi zote tuko tayari kushiriki na kuutekeleza kwa umakini na hasa kwa maeneo yote ambayo WAVIU tunayo nafasi na uwezo wa kufanya hivyo bila hata kuhitaji rasrimali za ziada. Kwa ujumla wake mkakati huu umetoa fursa kubwa kwa WAVIU kutoa mchango wao ili kuhakisha taifa linafikia malengo yake ya kutokemeza kabisa maambukizi mapya ya VVU, Kufuta kabisa vifo vitokanavyo na UKIMWI, na kufuta kabisa unyanyapaa na ubaguzi utokanao na VVU na UKIMWI. WAVIU, kupitia Baraza letu, tunaamini yote haya yanatekelezeka ikiwa kila mdau, kwa nafasi yake atatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Yote haya yanawezekana kwani kupitia mitandao na konga zake, WAVIU wanahusika na kusaidia kufuatilia na kutunza wagonjwa majumbani, kusaidiana na wafanyakazi wa afya kutoa unasihi na pia kuhusika na kutoa taarifa sahihi na kuelimisha jamii juu ya ufuasi salama na sahihi wa tiba ya UKIMWI, kujikinga na maambukizi ya VVU, kuhamasisha akina mama wajawazito pamoja na wenza wao kuhudhuria na kupata huduma za kuzuia maambukizi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto, kuhamasisha na kuhimiza kutetea na kupigania haki za makundi maalum kama vile wajane na yatima waishio na VVU.

Baraza pia limeanzisha majukwaa ya ushirikiano na Taasisi za elimu ya juu na utafiti, na Jukwaa la Wahariri wa habari TanzaniaMchakato huu unaendelea kwa Viongozi wa taasisi za dini, Sekta binafsina wadau wa maendelo ili kuhakisha malengo ya kitaifa dhidi ya UKIMWI yanafikiwa hasa katika kuondoa kabisa unyanyapaa. Yote haya yamewezakana kutokana na ushirikiano mkubwa wa wadau mbalimbali kupitia uratibu mzuri wa Tume ya Taifa ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), tunashukuru sana.

Mheshimiwa mgeni rasmi

Pamoja na mafanikio yote hayo, bado kuna changamoto ambazo zisipoangaliwa zinaweza kuwa ni kikwazo kikubwa katika kufikia malengo yote kama yalivyoainishwa kwenye kauli mbiu ya maadhimisho ya leo. Mathalani, pamoja na kuwepo unyanyapaa wa watu binafsi/ndani kwa baadhi ya watu wanaoishi na VVU, tafiti zinaonesha kwamba unyanyapaa dhidi ya wenye VVU kwenye jamii ni mkubwa sana na ndio chanzo kikubwa cha kukwama kwa jitihada zingine za kudhibiti UKIMWI. Kwa vile UKIMWI haubagui rangi, kipato, dini, aina ya kazi , makazi hata cheo cha mtu au nafasi yake katika jamii, ni dhahiri kuwa idadi ya wenye maambukizi ya VVU huwenda ikawa ni kubwa kuliko tunavyokadiria kuwa kwa sasa.

Mheshimiwa mgeni rasmi

Napenda kutoa rai kwa sekta zote za umma na binafsi, wafanyabiashara, viongozi wa siasa, , viongozi wa dini, taasisi za elimu ya juu na utafiti, na makundi mengineyo ya kijamii, tuhamasishane kupima afya zetu, na kwenda hatua moja mbele zaidi ya kuwa huru na nafsi zetu juu ya hali zetu kiafya baada ya kupima. Ombi hili pia nalielekeza kwa waajiri wote nchini kuweka taratibu zitakazowezesha kutoa elimu ya kujikinga na UKIMWI, huduma stahili za wale 4

 

wanaoishi na VVU na elimu dhidi ya unyanyapaa. Baraza lipo tayari kufanya kazi nanyi, tupeni nafasi. Tunaamini ni kwamba haya yatatoa msukumo mpya katika kuondoa unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya UKIMWI hapa nchini. Ni busara wakati wa kupima wanawake na wanaume waende pamoja, hii itapunguza Unyanyapaa na uonevu unaolenga wanawake wanaorudi nyumbani baada ya kupima na kwa nia njema kuwaeleza wenza wao kuwa wameonekana kuwa na maambukizi ya UKIMWI na kupigwa, kutengwa au kuachwa na wenzawao. Jamii ikemee jambo hili.

Mheshimiwa mgeni rasmi

Tunashukuru sana kwa serikali na wadau wengine kulitambua kundi la WAVIU na Baraza lake kupitia Sera na Mikakati yote ya UKIMWI ya Taifa. ; hata hivyo , pamoja na fursa hiyo kuwepo, hakuna mwongozo wowote ule uliopo wa kitaifa, unaolekeza namna ya Baraza pamoja na Konga zake kupata bajeti kutoka serikalini ili kuchangia uendeshaji wa shughuli za Baraza na wadau wake. Tunaiomba serikali, pamoja na halmashauri zake , waweke utaratibu wa kutenga bajeti na kutoa ruzuku kwa shughuli za Baraza ili kupunguza utegemezi kutoka nje wakati Baraza likiendelea kujenga uwezo wake wa kujitegemea, kwani WAVIU ni wadau muhimu sana katika kutekeleza mwitikio wa kitaifa wa masuala ya UKIMWI.

Lakini zaidi na muhimu sana , kilio chetu kwako, tunakuomba sana kwa heshima kubwa, Mheshimiwa Rais, kwa nafasi yako uliwezeshe Baraza kuwa na jengo lake lipate mahali pa kuendesha shughuli zake kwa amani na ufanisi zaidi kwani hadi sasa tunaishi kwenye majengo ya kupanga na mara nyingi imekuwa ni vigumu kulipa pango kwa muda muafaka na hivyo kuleta adha kwa wenye nyumba, kwani gharama za pango ni kubwa na zinapanda kila mwaka ambazo hatuwezi kumudu kwani baraza bado ni changa. Tunakusihi sana, tena sana utuwezeshe kwani tunahitaji kujitegemeza sasa.

Mheshimiwa mgeni rasmi

Ufuasi sahihi na kamili wa tiba itolewayo kwa WAVIU ni moja ya misingi ya kuimarisha afya, utu, ustawi na ari ya kuishi maisha bora bila unyanyapaa kwa wanaoishi na VVU katika jamii. Hata hivyo, hali hii haiwezi kufikiwa kama uhakika wa upatikanaji wa huduma za tiba, vifaa tiba na vitendanishi utakuwa ni finyu. Tunaiomba serikali, ituhakikishie uwepo wa dawa za kutosha, zenye ubora unaozingatia viwango vinavyokubalika, na kwa kila anayestahili huduma hiyo aipate kwa muda muafaka. Tunahitaji msukumo mpya ili kila yule anayesatahili kupata dawa apate kwa urahisi, , usawa na haki kwa wote

Mheshimiwa mgeni rasmi

Baraza na watu wote tunaoishi na VVU tunaamini kabisa mikakati iliyowekwa kwenye sifuri tatu inaweza ikawa jibu sahihi ya Tanzania bila UKIMWI inawezekana endapo tu wadau wote watathaminiwa, watashiriki na watashirikishwa katika mapambano hayo na kufanya yafuatayo 5

 

 

 Kila upande wa wadau tukianza na watu wanaoishi na VVU watafuata ufuasi sahihi wa dawa kwa ukamilifu na masharti ya kuishi na VVU wanayopewa na washauri nasaha.

 Watoa huduma nao watafuata maadili ya kazi zao kutowanyanyapaa watu waishio na VVU na kuona UKIMWI ni sawa wa magonjwa mengine ambayo wao wanatoa huduma.

 Wataalamu wanaoagiza dawa wanafuata maadili ya kazi zao kwa kuagiza dawa zenye ubora kwa tiba sahihi, kuagiza na kusambaza dawa kwa wakati sahihi, na kuepuka vituo kuwa na upungufu wa dawa mpaka ili kuondoa hofu watumiaji.

 Watunga sera, watoa maamuzi na vyombo vya habari kutokuwa na lugha za unyanyapaa ambazo zinawafanya watu wanaoishi na VVU kuogopa kujitokeza katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Kauli hizi ni hatari, kwani zinarudisha nyuma harakati za mapamabano dhidi ya UKIMWI. Tunakuomba uzikemee kauli na wale wote wanaotoa kauli hizi waache mara moja.

 

Mheshimiwa mgeni rasmi

Mafanikio ya utekelezaji wa maazimio yaliopitishwa na Umoja wa mataifa 2011 yanategemea ufanisi katika ushirikishwaji wa dhati wa WAVIU katika ngazi za maamuzi na utekelezaji wa sera na program wa mwitikio dhidi ya UKIMWI. Tunaomba serikali itoe mwongozo wa kitaifa kwa wadau wote, ngazi zote kuhakikisha watu wanaoishi na VVU wanashirikishwa katika kutoa mchango wao kwenye maamuzi yanayohusu masuala na maisha yao kwani kuna baadhi ya halmashauri nchini hazishirikishi watu wenye VVU katika kupanga, kutekeleza na kutathmini program za UKIMWI.

Mheshimiwa mgeni rasmi

Kwa kumalizika, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru wote waliyoiwezesha NACOPHA kufikia hadi hapa tulipo. Nitoe rai kwa wadau wote kushirikiana na kulitumia Baraza katika kuratibu, kutetea na kuwafikia WAVIU pale walipo katika mwitikio wa kitaifa wa shughuli za UKIMWI ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa(Sifuri 3) kuondoa unyanyapaa na ubaguzi, maambukizi mapya ya VVU na Vifo vitokanavyo na UKIMWI na kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyoanishwa ushirki wa WAVIU ufanyike ipasavyo.

 

Tanzania Bila unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya VVU na UKIMWI inawezekana

 

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

VITALIS VITUS MAKAYULA

 

Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na VVU Tanzania

  • COAT OF ARM
  • UNAIDS
  • USAID
  • TACAIDS
  • GLOBAL FUND
  • GNP


The National Council of People Living with HIV & AIDS in Tanzania (NACOPHA) Mbezi Beach Area, Block 'F' Plot no. 450/5 Mwai Kibaki Road, Kinondoni District, Dar es Salaam,Tanzania
Copyright © 2019 NATIONAL COUNCIL OF PEOPLE LIVING WITH HIV TANZANIA