Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI watahadharisha.

uploaded 09/06/2016

 

BARAZA la Taifa la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA), limeitaka jamii kutambua kuwa bado kunatatizo kubwa la ugonjwa huo kwani limeanza kusahaulika.

Aidha, baraza hilo limedhamiria kutoa elimu kwa jamii kuhusu maambukizi ya virusi vya UKIMWI ili kufikia malengo waliyojiwekea ifikapo mwaka 2030 ya kutokuwapo kabisa kwa maambukizi mampya.

Malengo hayo ni kumaliza unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI.

Hata hivyo, NACOPHA limesema malengo hayo hayawezi kufikiwa kama uhakika wa upatikanaji wa huduma za tiba, vifaa tiba na vitendanishi utakuwa mfinyu.

Mwenyekiti wa NACOPHA, Justine Mwinuka, alisema hayo alipokuwa akielezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na baraza hilo mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya UKIMWI.

Aliomba wadau mbalimbali likiwamo Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) pamoja na Serikali kuendelea kuwasaidia watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.

Alitoa rai kwa serikali ihakikishe kunakuwapo na dawa za kutosha za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs) zenye ubora na viwango vinavyokubalika na kwa kila anayestahili huduma hiyo aipate kwa muda muafaka.

"Tuna amini kabisa mikakati iliyowekwa na Serikali inaweza ikawa jibu sahihi la Tanzania bila UKIMWI inawezekana endapo tu wadau wote watathaminiwa, watashiriki na watashirikishwa katika mapambano hayo,'' alisema.

Aliwaomba watoa huduma za afya wafuate maadili ya kazi zao na kutowanyanyapaa watu waishio na virusi vya UKIMWI.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa NACOPHA, Deogratius Rutatwa, alisema licha ya Sheria ya UKIMWI kupitishwa na Bunge, lakini mpaka sasa haijaanza kutumika kwa madai kwamba miongozo yake haijawa tayari na kwamba Serikali imeshindwa kuwafikia wanaoishi na Virusi vya UKIMWI ili kujua matatizo yao.

 

 

  • COAT OF ARM
  • UNAIDS
  • USAID
  • TACAIDS
  • GLOBAL FUND
  • GNP


The National Council of People Living with HIV & AIDS in Tanzania (NACOPHA) Mbezi Beach Area, Block 'F' Plot no. 450/5 Mwai Kibaki Road, Kinondoni District, Dar es Salaam,Tanzania
Copyright © 2019 NATIONAL COUNCIL OF PEOPLE LIVING WITH HIV TANZANIA