Mdahalo wa wanajamii Kuhusu Mwitikio wa VVU na UKIMWI: Kufikia Malengo ya kitaifa ya Mwaka 2030.

Dar es Salaam,Tanzania- Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) kanda ya Dar es Salaam limefanya mdahalo wa wadau na kundi la wanaume kutoka mikoa ya Pwani na Dar es Salaam. Lengo la mdahalo huo lilikuwa ni kujadili na kuangazia mitazamo mbalimbali ya wanajamii juu ya changamoto na mikakati ya mwitikio wa VVU na UKIMWI.

Mdahalo huo ulilenga kubainisha makundi yaliyosahaulika au yasiyofikiwa vyema katika jitihada za kupambana na UKIMWI, pamoja na michango ya jamii katika kuongeza kasi na uendelevu wa mwitikio huo hadi kufikia malengo endelevu ya mwaka 2030.

Katika mdahalo huo, makundi kadhaa yaliyosahaulika yaligusiwa ambayo yanakabiliwa na changamoto kubwa katika kupata huduma na elimu kuhusu VVU na UKIMWI. Makundi haya ni pamoja na:
– Wafugaji ambao huishi kwa kuhama-hama, hivyo kupata ugumu katika kupata huduma za afya na elimu kuhusu VVU na UKIMWI.
– Wafanyakazi wa saluni za kiume ambao wanaweza kuwa katika hatari ya ushiriki wa ngono zembe.
– Wajidunga wanaoshirikiana mabomba ya sindano, hivyo kusababisha hatari ya kuambukizwa VVU.
– Wasichana wa kazi za majumbani ambao wanaweza kuwa katika hatari ya kushawishiwa kufanya ngono zembe na waajiri wao.
– Wanawake wanaojihusisha na biashara za ngono katika maeneo ya vijijini.
– Viongozi wa dini ambao wanahitaji elimu zaidi kuhusu sayansi ya VVU ili kuelimisha waumini wao kwa usahihi.
– Watu wenye ulemavu wa kusikia na kunena ambao wanakabiliwa na changamoto za kimawasiliano.

Katika kusaidia kasi na uendelevu wa mwitikio wa VVU na UKIMWI, jamii imekuwa na michango ifuatayo:
– Jamii ya watu wanaoishi na VVU imekuwa ikitoa elimu kuhusu VVU na UKIMWI kupitia vikundi mbalimbali na kongamano, pamoja na kushirikisha shuhuda binafsi.
– Kutoa mafunzo na ujuzi wa kujitegemea kwa watu wanaoishi na VVU, kama vile utengenezaji wa bidhaa na mbinu bora za kilimo.
– Kutoa msaada kwa wahitaji, ikiwa ni pamoja na chakula, sare za shule, na ada ya masomo.

Kutokana na mdahalo huo, kuna mapendekezo kadhaa yaliyotolewa ili kuimarisha mwitikio wa VVU na UKIMWI:
– Kuongeza uwezo wa kongamano ili kiweze kufikia watu wote katika vijiji na mitaa yote.
– Kuendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
– Kuhakikisha vituo vya huduma za VVU na UKIMWI (CTC) vinafanya kazi kwa muda wa saa 24 ili kuongeza upatikanaji wa huduma.
– Kuzingatia umuhimu wa usiri wa taarifa za wapokea huduma ili kupunguza utoro wa dawa.

Mdahalo huu umekuwa hatua muhimu katika kujenga mwitikio imara na endelevu wa VVU na UKIMWI nchini Tanzania. Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) likiwa linasherekea miaka 20 tangia uundwaji wake mnamo septemba 2 litafanya mdahalo wa kitaifa wenye lengo kuimarisha ubia na ushiriki wa jamii katika mwitikio endelevu wa UKIMWI Tanzania.Pia NACOPHA wanatoa wito kwa jamii nzima kushirikiana katika jitihada za kupunguza maambukizi mapya ya VVU na kuunga mkono watu wanaoishi na VVU ili kuwa na maisha yenye afya na ustawi.

About the Author

You may also like these